Sunday 12 August 2018

WASHAIRI CHIPUKIZI


Malenga Chipukizi wa Karne ya 21 katika Utungaji wa Mashairi Bora: Changamoto na Masuluhisho yake



Neema B. Sway
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
&
Eric F. Ndumbaro
Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge


Hali ya malenga wa Kiswahili katika miaka ya 1960 hadi 1990 ilikuwa tofauti sana katika suala la usukaji wao wa mashairi kifani na kimaudhui ikilinganishwa na wa miaka ya 2000 hasa katika kizazi cha karne hii ya sayansi na teknolojia. Katika miaka ya 1960, washairi wengi walitunga tungo zenye viwango vinavyokidhi jamii zao kiasi cha kuacha mwangwi usiofifia hata katika vipindi vilivyofuata. Mafanikio haya pengine yalifikiwa kutokana na sheria walizojiwekea ambazo ziliwaongoza katika utungaji wao wa mashairi. Kwa upande wao, malenga chipukizi wa karne hii, wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya kutunga tungo chapwa na zenye wepesi wa fani na mawanda ya kimaudhui. Je, ni changamoto gani zinazowafanya malenga chipukizi wa karne ya 21 kushindwa kupea katika kutunga tungo za Kiswahili zenye ladha, uzito, mvuto na ubora unaostahili? Je, ni masuluhisho yapi yatakayoweza kusaidia katika kukabiliana na changamoto hii inayowasonga malenga chipukizi wa karne ya 21? Hivyo basi utafiti huu unalenga kuchunguza changamoto zinazowakabili malenga chipukizi wa Kiswahili wa karne ya 21 na kupendekeza masuluhisho ili kufikia utungaji wa mashairi bora ya Kiswahili. Utafiti huu umekusanya data zake kwa njia ya usomaji wa maandiko mbalimbali ya kifasihi na kinadharia na majadiliano na wapenzi wa mashairi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii. Makala hii inatarajia kuchochea ubunifu wa uandishi wa mashairi kifani na kimaudhui kwa malenga chipukizi wa Kiswahili. Aidha, utafiti huu utahamasisha tungo zenye ladha, mvuto na ubora unaostahili kwa malenga chipukizi.

No comments:

Post a Comment