Thursday, 22 March 2012

WANAWAKE

Br. Gallus na Br. Eric

WANAWAKE NA MAENDELEO KATIKA MAADILI!

Je ni wapi tulikotoka, tulipo, tunapokwenda na tutakapokuwa?!! Waswahili wana methali isemayo kwamba “yaliyopita si ndwele tugange yajao” na “usiache mbacheo kwa msala upitao”. Ukijaribu kuziangalia methali hizi kwa jicho la kifalsafa hasa falsafa ya Kiafrika utagundua kuwa methali hizi mbili zipo katika kipengele cha muda katika falsafa ya kiafrika. Tukimtazama John Mbiti kama mwanafalsafa mmojawapo wa Kiafrika katika mkondo wa Ethnofilosofia amegawa dhana ya muda katika sehemu kuu tatu ambazo ni: Zamani, Sasa, na Wakati ujao.
Kwa mujibu wa methali zetu hapo juu tunaona kwamba, methali ya kwanza inaonesha kuwa wakati uliopita hauna thamani wakati katika methali ya pili inaonesha kwamba wakati wa zamani ni bora kuliko wakati ujao. Ni wazi kwamba kwa Mwafrika katika dhana ya muda hana wakati ujao isipokuwa ameiga tu kutoka katika mataifa mengine. Hii inajidhihisha hata katika vipengele mbalimbali vya fasihi ya Kiafrika, mfano visasili, ngano na hata hadithi nyingine za Kiafrika mara nyingi hueleza mambo ya wakati uliopita na si ujao. Je mipango ya serikali yetu ni ya muda mrefu?
Nadhani mpaka hapo tuko pamoja, kama ndiyo basi tujiulize hivi; je tulikotoka ndiyo si ndwele? Na vipi kuhusu tugange ya jao? yaani tunapokwenda na tutakapokuwa?, na msala upitao je, ndiyo tunakokwenda? Na vipi hiyo mbacheo je ndiyo tulikotoka? Pole kama nimeanza kukuacha ila usijali maana wapare wana methali  isemayo kuwa, “hata ng’ombe aliyeko nyuma hutimua vumbi”. Kwa hiyo naamini kuwa unajitahidi kunielewa japokuwa utachelewa.
Vilevile kuna mwanafalsafa mmoja wa kimagharibi, George Wilhelm Hegel. Katika “The ‘Philosophy of History” ameligawa bara la Afrika katika sehemu kuu tatu ambazo ni Kusini mwa jangwa la Sahara – ambayo ndiyo ameiita Afrika halisi, pia kuna Kaskazini mwa jangwa la Sahara na sehemu ya tatu ni Maeneo ya Mto Nile. Mwanafalsafa huyu alikataa katakata kumuongolea mwafrika kutokana na sababu zifuatazo: kwanza alisema kuwa, mwafrika ni mtu ambaye hana akili, historia, maendeleo, utamaduni, matukio, hana dini na wala hana maadili. Je ni kweli?
Kwa kweli naomba nieleweke tangu mwanzo kwamba nia yangu si kutonesha majeraha tuliyoyapata enzi za mkoloni ila ni kutaka kuangalia namna mawazo yao yanavyoweza kuhalisika katika ulimwengu huu wa maendeleo. Sasa basi hebu tujipe wasaa kwa kuangalia suala zima la maadili na ulimwengu wa maendeleo.
Awali ya yote ingefaa tuangalie mitazamo mbalimbali juu ya dhana hii ya maadili. Mihanjo (2004:247) anasema kuwa, “sharia za kimaadili huibua mashaka”, anaendelea kufafanua kuwa,
“…mawazo ya kimaadili pamoja na vitu tuvionavyo yapaswa kuingizwa kwenye uwanja wa mashaka. Watu katika jumuiya mbalimbali wana mawazo tofauti juu ya nini chema na sahihi. Desturi na sheria hutofautiana kutoka jumuiya moja hadi nyingine na katika jumuiya ileile watu hutofautiana katika nyakati tofauti”.
Huu ni mtazamo wa kifalsafa unaongalia uwepo wa kitu kama kinavyoonekana (appearance) na uwepo wa kitu kama kilivyo (reality). Lakini pamoja na hayo tunaamini kwamba Mwafrika anafuata zaidi mila na desturi za jamii yake pamoja na kwamba zinatofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Na kwa kuwa watu hutofautiana kulingana na nyakati tofauti lakini maadili hayabadilika kulingana na nyakati ila watu ndiyo wanaobadilika kulingana na nyakati na kuanza kupuuzia na kuyaacha maadili mema.
Kwa kiasi kikubwa nakubaliana na mwanafalsafa Jonh Samuel Mbiti katika “African Religious and Philosophy”  (1960) yeye anaona kwamba, tangu zamani Mwafrika ni mtu wa dini na hawezi kujitenga na dini yake kwani kwa Mwafrika kujitenga na dini ni kujitenga na jamii kwa sababu kila kitu kwa Mwafrika ni dini. Hivyo basi hatuna budi kutazama dhana ya maadili katika mtazamo wa kidini kwa kuwa kila kitu kwa Mwafrika ni dini.
Dhana ya Maadili: Maana yake ni nini?
Kwa mujibu wa Akhweso, H. huyu ni Padre wa kanisa katoliki, amejaribu kufalisi dhana ya maadili katika mtazamo wa kidini kama ifuatavyo; 
“Maadili ni wema wa mwenendo au tendo la mtu; ni kule kuhukumiwa kwa mwenendo wa mtu kuwa ni mwema, au tendo la kibinadamu kuwa ni jema. Mwenendo au tendo la mtu ni jema vinapolingana na hadhi yake kibinadamu, yaani vinapoakisi utu wake. Hapa tunasema mtu huyu ni mwadilifu, au tendo hili ni adilifu. Na mwenendo wa mtu au matendo yake vinapokuwa kinyume na hadhi yake ya kibinadamu, yaani kinyume cha utu wake, tunahukumu kuwa ni mabaya, na huo ni ukosefu wa uadilifu. Kwa kifupi, uadilifu ni wema wa mwenendo au tendo la kibinadamu, na ukosefu wa uadilifu ni ubaya wa mwenendo au tendo la kibinadamu. Maadili pia ni taaluma juu ya kanuni zinazohukumu mwenendo na matendo ya mtu kulingana na UTU wake”. Anaendele kufafanua kwamba,
“Katika kuhukumu uadilifu wa mwenendo au tendo la mtu (yaani, wema au ubaya wao), dhana ya maadili inazingatia vipengele vifuatavyo (ambavyo vinafafanua dhana nzima ya maadili):
A) Sheria ya kimaumbile ya Kimaadili: Hii ni sheria iliyochapwa katika nafsi ya binadamu tangu kuumbwa kwake. Tunaiita ‘sheria’ kwa kuwa hutoa mwongozo na hukumu juu ya uadilifu wa mwenendo na matendo ya mtu kulingana na utu wake; ni ya ‘Kimaumbile’ kwa kuwa mtu aliumbwa nayo, si kitu ambacho mtu anatunga bali iko katika hulka yake ya kibinadamu; ni ya ‘kimaadili’ kwa sababu inahusu wema au ubaya wa mwenendo na tendo la kibinadamu. Sheria hii inasema: “Tenda wema, epuka ubaya.” Binadamu huitambua na/au huing’amua sheria hii ya kimaadili kwa kutumia vipawa vyake vya akili na utashi. Vipawa hivi ndivyo vinavyomtofautisha mwanadamu na viumbe vingine vyote katika ulimwengu huu, na pia humpa hadhi ya juu na mamlaka ya kuvitawala viumbe hivyo.
Kwa kutumia kipawa cha akili binadamu hutafuta, hung’amua na kufahamu ukweli. Kipawa cha akili hutuwezesha kufahamu au kujua jambo fulani, na tunafahamu au kujua jambo lililo la kweli. Mtu anapojiuliza kama jambo fulani ni la ‘kweli au la,’ au kama ‘lipo au halipo,’ anatumia kipawa cha akili. Ukweli ni lengo kuu la kipawa cha akili. Na akili inapokosa ukweli, huwa na mahangaiko makubwa na maswali mengi; lakini inapopata ukweli, hutulia kwa kuwa imeridhika. Chakula kikuu cha akili ni ukweli, hivyo kila mmoja, kimaadili, anao wajibu wa kuilisha akili yake kwa kutafuta ukweli daima, yaani, kujifunza.
Utashi ni kipawa kinachotuwezesha kuona jambo fulani kuwa ni jema. Na jambo lililo jema ni lile ambalo akili imethibitisha kuwa ni la kweli. Akili inapoona kuwa jambo fulani ni kweli utashi huliona kuwa ni jema; lakini akili ikiona kuwa si la kweli, utashi huliona jambo hilo kuwa baya. Kwa kuwa utashi huhukumu jambo fulani kuwa ni jema au baya, ndicho pia kipawa tunachotumia katika kutoa uamuzi: ama kutenda au kutotenda, ama kuchagua hili au lile. Utashi daima hutenda au kuchagua lile lililo jema, na huacha au kutolichagua lile lililo baya. Utashi ukiona jambo fulani kuwa ni baya, kamwe hautaamua kulitenda. Hivyo,mtu mwenye akili timamu hawezi kuamua kutenda uovu wowote (mf. Ujambazi), kama akili yake inaona kuwa kitu hicho si sawa, maana utashi utaona kuwa ni kibaya, na hivyo utaamua kutolitenda. Ni pale akili itakapokuwa na sababu za kutosha za kuona kuwa tendo hilo ni halali (hata kama ni ovu), ndipo utashi utaona kuwa ni jema, na hivyo mtu huamua kulitenda.
Mpaka hapa tumeona jinsi sheria ya maumbile ya kimaadili ilivyo katika vipawa vya akili na utashi, ikiviongoza vipawa hivyo kumwezesha binadamu daima “kutenda wema na kuepuka ubaya.” Mtu anapotumia vipawa hivyo kwa kuzingatia sheria ya maumbile ya kimaadili, anatenda kwa kadiri ya hadhi yake ya kibinadamu, hivyo anakuwa mwadilifu. Kwa kuishi na kutenda kadiri ya hadhi yake, binadamu hujipambanua na viumbe vingine: wanyama, mimea, mawe, n.k. Hadhi yake ya kibinadamu inamdai daima kujipambanua na viumbe hivyo. Hii inabainisha wazi kuwa kuishi kimaadili si jambo la hiari bali ni la lazima kwa mujibu wa hadhi yetu ya kibinadamu. Kule kuumbwa na utu (yaani, kuwa mtu), ndiko kunakomdai mtu kuwa mwadilifu, madai ambayo hawezi kuyakataa maadam ni mtu. Kuwa au kutenda kinyume na utu ni kujishusha hadhi yetu na kuwa sawa na, au hata kuwa chini ya wanyama”.
Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, je hawa watu wanaokwenda kinyume na maadili inamaana kwamba hawana akili wala utashi?! Nachelea kusema ingawaje ndivyo ilivyo kwa mujibu wa mtazamo huu wa kidini kwamba watu wanaokiuka maadili wanaonekana hawana akili wala utashi na nidhahiri kwamba hata dhamiri zao ni kama panga butu lililojaa kutu.
Nasema haya kwa masikitiko makubwa sana, hasa ninapowaona dada zangu jinsi wanavyotengeneza maumbile yao kwa madawa ya kichina na namna wanavyovaa siku hizi. Je, kweli hiyo ni akili au matope?!! Nina hakika na nina imani kuwa siku zote Mungu hafanyi makosa katika kazi zake, na ndivyo anavyopenda tuwe kama alivyotuumba. Lakini kutokana na ujinga wetu tumeanza kujibadilisha na kutaka kufanana na wazungu. Je hayo ni maadili ya Kiafrika?!
Kwa kweli sijawahi hata siku moja kusikia wala kuona Mzungu, Mchina, Muhindi, Mwarabu nk. anataka kubadili rangi yake na kuwa mweusi, au macho yake yawe kama yetu, au makalio yake, au nyusi zake ziwe kama zetu!! Mambo haya mmetoa wapi dada zangu?! Mbona Wachina wenyewe hawatumii hizo dawa wakati mazingira ya makalio yao tunayaona!! Labda kutokana na “uzero grazing” wangu ndiyo maana sijaona basi naomba mnisamehe na mnijuze ili nami nifunguke.
Nadhani tupo wengi sana kama siyo wote ambao tunachukia sana tabia hii ya dada zetu kutembea nusu uchi kama siyo uchi kabisa. Mara nyingi utaona wakinadada wengi wamevalia vipensi huku mapaja yote yako nje!! Je hii ni nini!! Keep your eyes down, najua huu ni msemo wa wanafalsafa lakini hauna akili kabisa katika mambo kama haya ya kimaadili.
Ni jambo la ajabu na kusikitisha kuona kwamba hata zile nguo ambazo tulifundishwa kwenye jando na unyago kuwa hazipaswi kuonekana hadharani siku hizi ni jambo la kawaida sana kuona zinavaliwa nje, mfano: tight, chupi, vipedo, nk. Je haya ndiyo maendeleo ya kimaadili au? Ah! samahani inawezekana ndiyo kile mnachokisema kwamba, “wanawake tunaweza” Kama ni hivyo nami nakubaliana nanyi tena kwa asilimia zote kwamba, wanawake mnaweza kuiga.
Siku zote watu kama hawa, mimi huwa napenda kuwafananisha na mwandawazimu ambaye ni chizi kama si mwehu au zuzu. Nasema hivi kwa sababu mwandawazimu au chizi ndiye anayeweza kuvua nguo zake na kuweka begani kisha akajisitiri kwa viganja vya mikono yake sehemu zake za siri halafu maisha yakaendelea kama kawaida. Je naongopa?
Mtaniwia radhi dada zangu, sina ugomvi nanyi bali ninapenda kuwaonesha kuwa mambo mnayoyafanya ni aibu tupu kwa wazazi na wadogo zenu, pia hata kwa wageni. Labda mtaniuliza wageni gani hao?
Siku moja rafiki yangu kutoka ng’ambo alikuja kunitembelea, basi katika kumtembeza tembeza hapa na pale katika jiji letu la Dar es Salaam kwa lengo la kujionea jinsi Tanzania ilivyo, aliniuliza swali ambalo inaonesha aliwaza na kuwazua kwa muda mrefu sana mwishowe yakamshinda. “hivi kwa nini watanzania wengi hususani wanawake wanapenda kuweka nywele ndefu kama za kwetu? halafu wengi wanapenda kuchubua ngozi zao na kuonekana weupe! Ni kwa nini?”. Moyo wangu ulikuwa ukinidunda maana nilifikiri atagusia suala la makalio, kwa kweli nilishukuru Mungu nikakumbuka ile methali isemayo “mwenye macho haambiwi tazama”. Kwa kweli nilijiumauma sana katika kujibu maswali yake maana ni mambo ya aibu hata kuelezea. Mwisho akaniambia kuwa, “unajua sisi wazungu hizi nywele ndefu zinatupa shida sana, kwani kila wakati inabidi kutikisa kichwa ili zikae vizuri na wakati mwingine tunaamua kuzifunga kwa nyuma kusudi zisitusumbue”, Akaendelea kusema kwamba, “mimi natamani sana kama ningekuwa na nywele kama zenu, kwani ningeondoa kabisa usumbufu tena ningeokoa fedha nyingi sana, maana hizi nywele zetu ni gharama sana kuzitunza”.
Aibu ilizidi kuongeza kwani kila tulipokuwa tukitembea tulipishana dada zetu na mama zetu wakiwa na wamevalia nguo za ajabu ajabu na wengine wakiwa nusu uchi. Pia asilimia kubwa walikuwa na nywele za katani. Kweli haya ni maendeleo, wanawake mnaweza!
Kadiri siku zinavyokwenda asilimia kubwa ya wanawake/wasichana wanazidi kuwa “artificial” (made as a copy of something natural) au tunaweza kusema wanakuwa maroboti, kutokana na kwamba sehemu nyingi za viungo vyao vimeweza kufanyiwa “modification” (the action of modifying – a change made) na kuonekana bado vipo kwenye chati. Mfono: kope, mboni za macho zenye rangi mbalimbali, makalio, kucha, matiti/maziwa nk.
Siku hizi kuna jeki maalum za kuinua matiti kutoka ulalo kwenda wima na hata kuyafanya yaonekane madogo zaidi. Mambo haya yote ya nini dada zangu!. Mmesahau ile adhabu Mungu aliyowapa babu zetu, ile adhabu ya Sodoma na Gomora. Maana ilikuwa ni mambo kama haya haya ya kutaka kumrekebisha Mwenyezi Mungu na kumuonesha kwamba amefanya makosa katika uumbaji wake.
Jambo linalonishangaza zaidi ni kwamba hata serikali yetu haioni mambo kama haya kuwa ni hatari kwa Taifa tena Taifa lenye watu maisikini kama Tanzania. Tafiti nyingi zinaonesha kwamba mambo haya yote yafanywayo na wanawake/wasichana yana madhara makubwa sana kiafya, kwani huweza kusababisha saratani za aina mbalimbali na kuliongezea mzigo Taifa. Ndiyo maana nasema serikali haipaswi kufumbia macho mambo kama haya yasiyo na tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Pia kwa upande mwingine mambo kama haya hatupaswi kuiachia serikali peke yake kwani hili ni jukumu la kila mwenye akili, utashi na busara. Vilevile hata wanaharakati mnapaswa kukemea uchafu huu, kazi yenu siyo tu kung’ania kukosoa serikali na kudai haki sawa huku mkiacha maadili yakiporomoka. Amakweli! huku ndiko kuweza, na kwa kweli mnaweza tena bila hata kuwezeshwa maana…
                                Ya Ulaya mmeiga, bila hata kuwezeshwa, 
                             Ya nini kulalamika, kutwa kucha redioni,
                                    Wanawake twanyanyaswa, hamchoki kulalama,
                                Nani kawalazimisha, uchi nusu kutembea.
                        Wapi wanaharakati, maadili kutetea,
                       Sijifanye hamnazo, uuzo kuufumbia,
                               Mmeng’ang’ania siasa, viongozi kukosoa,
                                   Nashangaa nashangaa, hata Nkya hayaoni.
                      Wanaharakati gani, mso jali maadili,
                             Hakika mnanikera, kutwa kucha siasani,
                                   Mwanahakati popote, hata kwenye maadili,
                             Nashangaa nashangaa, hata hili hamjui.

Poleni kwa kuwachanganyia tanzu, kweli hizi zote ni hasira maana nimekereka mpaka nikaamua kuimba ili kuonesha hisia zangu juu ya uozo huu.

Kama tunavyojua sarafu iliyohalali ni ile iliyo na pande zote mbili, hivyo haitakuwa jambo la burasa kama sitageuza upande wa pili nakujionea uhalali wa sarafu hiyo, maana siku hizi si jambo la ajabu kusikia shilingi ya kichina hiyo. Maana tumetoka kwenye Uarabu na Uhindi na sasa tupo kwenye Ukameruni. Nijambo la kisikitisha sana tena sana kwani siku hizi vijana wengi wa kiume wanajihusisha na masuala ya urembo!, kama vile, kutoga masikio na kuvaa hereni, kujipodoa kama dada zetu, kusuka nk.
Lengo hasa la kufanya haya yote kwa vijana wa kiume ni nini? Kama siyo kujiingiza katika ukameruni (ushoga). Marembo haya kwa wanaume yanaleta tafsiri mbaya sana. Nashangaa kuona jamii inawapokea watu kama hawa na kuwachukulia kana kwamba jambo walifanyalo ni la kawaida na limezoeleka katika jamii yetu. Napenda kuipongeza serikali yetu kwa kuliona hili na kulikemea kwa nguvu zote, hivyo jamii nayo kwa kufuata mfano wa serikali inapaswa kukemea zaidi vitendo vya uvunjifu wa utu au ubinadamu, kwani jamii ndiyo inayowazaa wapumbavu kama hawa.
Mambo yakuishia hapo tu, kwani hali inazidi kuwa mbaya zaidi na hii ndiyo hofu yangu kubwa na sijui kama itapatiwa uvumbuzi wa hara, maana; ni aibu kumuona kijana wa kiume tena msomi wa chuo kikuu anaacha makalio nje au anaonesha chupi nje! Mtu ambaye jamii nzima inamtegemea awe kiongozi. Unafikiri atakapokuwa kiongozi anaowangoza watakuwaje?! Niliwahi kumuuliza rafiki yangu mmoja nini maana halisi ya kuvaa “Kata K?” jibu alilonipa kwa kweli sikutegemea kama kweli hawa wanaoacha matako nje ndivyo wanavyoelewa! Aliniambia kwamba, maana yake ni “Usela Mavi” yaani hawa ni wasela mavi. Kwa kweli sikutamani tena kuendelea kufafanuliwa maana nilihisi tunapoelekea ni kubaya zaidi.
Najua wataalam wa falsafa (Critical Thinking and Argumentation) wataniambia kwamba kama hupendi kuona keep your eyes down, sawa kabisa. Je mtoto wako kifanya mambo kama hayo will you keep your eyes down? Hii haina akili hata kidogo katika suala zima la maadili, kwani mmomonyoko wa maadili haupaswi kufumbiwa macho vinginevyo tutatengeneza jamii ya wandawazimu.  
Hivyo hawa wote wanaokwenda kinyume na maadili mimi nawaona kama wandawazimu waliowehuka. Maana siku zote mwandawazimu huvua nguo na kutundika begani kisha hujisitiri na viganja vya mikono yake. Je kunatofauti gani kati ya vitendo vya mwandawazimu na wanaume mashoga au wanaovalia suruali chini ya matako? Je huku siko kutembea uchi?
                            Acheni ulimbukeni, kuiga msoyajua,
                                                 Ni sawa na limbukeni, alodandia kwa mbele,
                                          Ona sasa hana meno, yote sita sebuleni,
                               Achani usela mavi, kuiga msovijua.

                              Nani kakuambieni, mna matako mazuri,
                                       Hakiki nawaambiea, hilo ni changa la macho,
                              Nani amewaambia, chupi zenu zavutia,
                                    Huyo amewalisheni, tena matango ya pori.
Nadhani wale wenye utashi, akili timamu pamoja na busara watakuwa wamenielewa vilivyo, pia hata kinyume chake ni sahihi. 

1 comment:

  1. Just Keep your eyes down. Lakini pia hongera kwa kua mzalendo halisi, harakati zako ni za maana na ingekuwa vema ukawa kivitendo zaidi. God bless you bro.

    ReplyDelete