Friday 13 September 2013

FASIHI YA WATOTO NA VIJANA



NI VIGUMU KUWEKA MIPAKA DHAHIRI KATI YA FASIHI YA WATOTO NA VIJANA NA YA WATU WAZIMA.
Ni vyema kuanza kufafanua maana za maneno mbalimbali ya msingi yaliyojitokeza katika kauli hii kama vile: maana ya fasihi kwa ujumala, maana ya fasihi ya watoto na vijana, maana ya fasihi ya watu wazima pamoja na maana ya mipaka. Baada ya hapo kiini cha mada, ambapo tutaona ukubalifu wa hoja, kisha zitafuata sababu zinazoonesha ugumu wa kuweka mipaka dhahiri kati ya fasihi ya watoto na vijana na ya watu wazima.
Mulokozi (1996) anafafanua kuwa fasihi ni sanaa ya lugha inayoangalia maisha na mazingira halisi ya mwanadamu kwa kutumia lugha na maandishi
Kwa mujibu wa Ngure (2003:1) fasihi ni aina ya sanaa ambayo wasanii wake huonesha ustadi wao katika kutumia maneno kisanaa ili kuwasilisha ujumbe wao kwa wasomaji/jamii iliyonuiwa.

Pia Mulokozi (ameshatajwa) akimnukuu Egletoni (1983:20-21) fasihi ni sanaa ya lugha yenye ubunifu bila kujali kama imeandikwa au la.
Vilevile Nkwera (1978) anafafanua kwamba, fasihi ni sanaa yaani mkusanyiko wa kazi mbalimbali zilizosanifiwa kwa kutumia lugha itumiayo zaidi maneno, na kujishughulisha na jinsi binadamu anavyojitambulisha mwenyewe binafsi, pia anavyoathiriwa na binadamu wenzake aidha na viumbe vingine aina kwa aina katika mazingira mbalimbali ya maisha.
Hivyo kutokana na fasili hizo, kwa kifupi maana ya fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha katika kufikisha ujumbe kwa hadhira husika.
Wamitila (2003) anafafanua fasihi ya watoto kuwa ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto. Hii ni fasihi ambayo ni tofauti na ngano au hurafa.
Hivyo fasihi ya watoto na vijana ni kazi ya sanaa inayotumia lugha ilikufikisha ujumbe kwa watoto na vijana ambao wanaumri chini ya miaka 18.
Fasihi ya watu wa zima ni kazi ya sana inayotumia lugha ilikufikisha ujumbe kwa watu wenye umri juu ya miaka 18.
Kamusi ya kiswahili sanifu (2004) inafafanua maana ya mpaka kuwa ni mahali ambapo kikomo cha kitu na kingine.
Hivyo dhana ya mpaka inaweza kufasiliwa kuwa ni dhana inayoonesha mwachano baina ya kitu kimoja na kingine. Kwa mfano, inaweza kuwa mpaka kati ya nchi na nchi au eneo moja na jingine na hata kitu kimoja na kingine.
Ni kweli kabisa kuwa ni vigumu kuweka mipaka dhahiri kati fasihi ya watoto na vijana na fasihi ya watu wazima. Na hii inatokana na sababu za mwingiliano katika vipengele mbalimbali kama vile:
Muundo wa matini. Katika fasihi kuna miundo mbalimbali, kwa mfano, muundo changamani, muundo sahili na muundo rejea. Hivyo basi, ni suala la kawaida kukuta muundo wa moja kwa moja ambao ndiyo msingi wa fasihi ya watoto na vijana katika  fasihi ya watu wazima. Kwa mfano, riwaya ya “Vuta N’kuvute” ya Shaffi Adam Shaffi visa vyake vimepangangwa kwa mtiririko wa moja kwa moja.
Wahusika na uhusika. Hoja hii inajitokeza katika fasihi zote mbili yaani fasihi ya watoto na vijana na fasihi ya watu wazima, ambapo kwenye fasihi ya watoto na vijana kuna wahusika ambao ni watu wazima wenye kuvaa uhusika wa watoto yaani sehemu ambapo ilitegemewa awepo mhusika mtoto anawekwa mtu mzima, kadhalika kwa upande wa fasihi ya watu wazima hali hii hujitokeza pia. Kwa mfano katika tamthiliya “Wala Mbivu” ilipoigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1971 ambapo wahusika walioigiza walivaa uhusika wa watu wazima, mfano, wapo walioigiza kama baba, mama, mjomba, na shangazi,
Matumizi ya fantasia. Fantasia ni hali ya kuwepo kwa mambo ya ajabuajabu katika kazi ya fasihi yasiyotarajiwa kutokea katika maisha ya kawaida. Hali hii inajitokeza katika fasihi zote mbili yaani fasihi ya watoto na vijana na fasihi ya watu wazima. Kwa mfano katika tamthiya ya “Kivuli Kinaishi” matumizi ya fantasia yametumika kwa kiasi kikubwa ambapo ilitegemewa dhana hii ijitokeze katika fasihi ya watoto na vijana ambayo ni moja ya sifa kuu ya kazi hizo. Hivyo ugumu unajitokeza katika kujua fantasia ni dhana ya watoto au watu wa wazima.
Mwingiliano katika usomaji. Mara kwa mara wasomaji wa kazi hizi huingiliana yaani unakuta kazi zinazohusu watoto husomwa na watu wazima halikadhalika kazi za watu wazima husomwa na watoto. Hii inatokana na kutokuwepo kwa maktaba za kutosha za kazi za watoto. Pia hali hii inasababishwa na kukosekana kwa sheria zinazoweka mipaka kati ya kazi hizi. Hivyo inakuwa vigumu kuzuia mwilingiliano huu.
Mwingiliano katika mtindo. Mara nyingi baadhi ya vipengele vya kimtindo vya fasihi ya watoto na vijana hujitokeza hata katika fasihi ya watu wazima. Kwa mfano, matumizi ya picha mbalimbali zenye kufafanua maelezo ya mwandishi hujitokeza katika fasihi zote mbili. Mfano, katika riwaya ya “Mfadhili” ya Hussein Tuwa, pamoja na tamthiliya ya “Aliyeonja Pepo” ambazo ni fasihi za watu wazima waandishi wametumia picha mbalimbali katika kuelezea visa vyao. Hivyo matumizi ya picha pamoja na michoro ni kipengele muhimu katika fasihi ya watoto na vijana ambacho huwasaidia watoto kuelewa zaidi na kuvutiwa.
Vilevile uwepo wa matumizi ya taharuki. Dhana hii ina maana kwamba ni hali ya wasomaji kuwa na mshawasha wa kutaka kujua ni kitu gani kitafuata katika mwendelezo wa kisa. Dhana hii hujitokeza katika kazi zote mbili, hivyo inaleta ugumu katika kujua dhana hii inaangukia wapi kati ya fasihi ya watoto na vijana au fasihi ya watu wazima.
Kadhalika ni vigumu kubaini mawazo au falsafa ya mtunzi. Hii ni kutokana na kwamba kazi nyingi za kifasihi hutungwa na watu wazima zikiwemo pia kazi za watoto na vijana. Hivyo  kuna kuwa na mwingiliano mkubwa wa mawazo na kushindwa kubaini yapi ni mawazo ya watoto na yapi ni ya watu wazima.
Hivyo basi ili hali hii ya mwingiliano iweze kuepukika ni dhahiri kwamba kunahitajika kuwepo kwa sheria madhubuti na zenye kutekelezeka zitakazo dhibiti kazi hizi mbili zisiweze kuingiliana, hasa kwa watunzi na wasomaji. Kwa mfano watunzi wa fasihi ya watoto na vijana wajikite katika fasihi hiyo tu na watunzi wa fasihi ya watu wazima wajikite katika fasihi ya watu wazima tu na wala kusiwepo na mwingiliano wowote wa vipengele ili kuwapa urahisi wasomaji kujua mipaka ya kazi hizo.
MAREJEO.
Nkwera, F.V. M. (1978), Sarufi Fasihi: Uandishi wa Vitabu Sekondari na Vyuo. Tanzania publishing House. Tanzania.
Ngure, A. (2003),FasihiSimulizikwaShulezaSekondari. Nairobi. Phoenix Publisher.
OUP (T). Ltd. East African & TUKI. (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la pili). Oxford University Press (T). Ltd.
Mulokozi, M.M. (1996), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Taasisi ya Uchungu wa Kiswahili. Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2003), Kamusi ya Fasihi na Nadharia. Focus Publication Ltd. Nairobi-Kenya.

5 comments: