Monday 2 December 2013

NENO


FASILI YA NENO
Makala haya yana jadili fasili ya neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, ugumu wa fasili ya neno na kiini cha utata huo. Katika kujadili hayo makala yatagawanywa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza itaelezea maana ya neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, Sehemu ya pili tutaelezea kiini cha ugumu huo, na sehemu ya tatu tutatoa hitimisho.
Mdee (2010:5) hueleza kwamba dhana ya neno ina utata, kwani ni umbo lenye sura nyingi, utata huo hutokana na mitazamo tofauti ya wanaisimu, kuhusu kipashio hiki kitahajia (jinsi linavyo andikwa), kimatamshi na kimaana.
TUKI (2009) Hueleza kuwa neno ni kipashio cha usemaji ambacho hujengwa na mwandamano au mkuroro wa sauti zilizopangika kisilabi na ambazo hutambuliwa na wasemaji wa lugha inayohusika, kuwa kitu kimoja chenye maana mahususi.
TUKI (2010) Huelezea kuwa neno ni sauti au mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa pamoja na kuleta maana

Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa) hueleza kuwa neno ni mfululizo wa herufi zilizo fungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu. (Mdee, amekwishatajwa)
Kwa upande wake Cruse (1986:3) kama alivyo nukuliwa na Mdee, husema kuwa neno ni kipengele kidogo kabisa cha sentensi ambacho kinaweza kuhamishwa kutoka nafasi moja kwenda nyingine bila kuathiri sarufi ya lugha katika sentensi hiyo.
Vilevile neno huweza kuelezewa kama kipashio cha lugha,kinachowakilisha taarifa kama vile , matamshi, maana, tabia za kimaumbo na za kimuundo (Spencer, 1991)
Kiini cha ugumu wa kufasili neno
Zipo njia kadha za kisarufi ambazo zinaweza kutumika katika kuelezea dhana ya neno na katika kugawa mipaka ya maneno, miongoni mwa njia hizo ni, neno kama kipashio cha maana, neno kama kipashio cha kifonetiki au kifonolojia na neno kama kipashio huru na kisicho gawanyika (Rubanza, 2010). Ni vigumu kuwa na fasili toshelevu ya neno, sababu kubwa au kiini cha....
ugumu huo ni kutokana na vigezo tofauti vinavyo tumika katika kulifasili neno ambavyo hutupa maana tofautitofauti, vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;

Maana ya neno kiothografia, kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni maandishi yanayo acha nafasi mwishoni, neno hudhihirika linapokuwa katika maandishi tu na lisiwe na nafasi katikati, kwa mfano, meneno ambatano kama vile; bwana-misitu, bata mzinga, tahajia kama hiyo huchukulia kuwa ni maneno mawili bila kuangalia kuwa maneno haya yana dhana moja. Rubanza (ameshatajwa) hueleza kwamba neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati
Matatizo ya kigezo hiki
Hushidwa kuelezea maneno ambatani, kwao uandikaji wa neno ambatani kwa kutenga au kuacha nafasi katikati huchukulia kuwa ni maneno mawili. Hii sio sahihi kwani maneno ambatani huwa na dhana moja hivyo hutakiwa kuchukuliwa kama neno moja.
Kigezo hiki kina dhima ndogo katika uchambuzi wa kisarufi, hujihusisha tu zaidi katika namna ya kujifunza kuandika lugha(Rubanza, ameshatajwa) T.Y. Kigezo hiki hakijihusishi na lugha ya maongezi ambayo ndiyo inayotupa lugha ya maandishi.
Tatizo lingine ni kwamba zipo lugha ambazo hazitengi maneno yake katika uandishi wake, swali ni kwamba hapa utafasili je neno? Kwa mfano lugha kama Kigreenland “uluminippuq” maana yake, yumo (mwanaume) ndani ya nyumba yake, haya ni maneno mengi yaliyowekwa pamoja. Hapa kigezo hiki ni vigumu kufanya kazi.
Dhana ya nafasi tupu huonekana katika maandishi tu, tunapozungumza nafasi hizo tupu hazionekani au kujidhihirisha, sasa je neno liko kimaandishi tu?
Neno kifonolojia, huchukulia kwamba neno ni kipande cha lugha kinachotokana au kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi, kufuatana na vigezo fulani vilivyo wekwa ambavyo hutofautiana kutoka lugha moja na nyingine. Rubanza (ameshatajwa) hueleza kwamba zipo lugha ambazo upo uwezekano wa kulitambua neno kwa kutumia sifa za kimatamshi. Lugha kama hizi ni zile ambazo zina utaratibu wa kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno wakati wote. Hueleza zaidi kwamba sehemu hiyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila silabi ya kwanza ya neno, ua silabi ya pili toka mwisho kwa baadhi ya lugha. Kwa mfano katika lugha ya Kingereza;
“The rest of the books’ll have to go there,” mgawanyo wa maneno ni kama ifuatavyo; [the rest] [of the books’ll] [have to] [go] [there]. Hapo tuna mikazo mitano, inayoangukia katika; rest, boks, have, go na there, kwahiyo hapa tuna maneno matano ya kifonolojia.
Katika lugha ya Kiswahili mkazo huwa katika silabi ya pili kutoka mwisho, kwa mfano; anacheza, mkazo upo kwenye “che”.
Matatizo ya kigezo hiki
Kwa baadhi ya lugha, hasa Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu mkazo huhama kadri maneno yanavyoongezeka kwenda kulia katika tungo. Kwa mfano;
(a)    Baba
(b)   Baba analima
(c)    Babaanalima shambani
Neno la kwanza mkazo msingi upo kwenye “ba” ya kwanza , neno la pili mkazo msingi umehamia kwenye “li” na neno la tatu mkazo msingi umehamia kwenye “mba” Swali ni je kama neno katika  kigezo hiki cha kifonolojia tunaangalia mkazo msingi , haya maneno ambayo mkazo wake huhama sio maneno tena?
Tatizo lingine ni katika lugha ya Kingereza ambapo utengaji wa maneno kifonoloja huonekana kuwa mgumu, kwani neno moja kifonolojia kimaandishi huweza kuonekana kama maneno mawili au zaidi. Vilevile  maneno mengine yenye dhima za kisarufi hayapewi mkazo, bali hutegemea maneno yanayo ambatana nayo, kwa mfano maneno kama vile; her, it, that, yakisimama yenyewe hayapewi mkazo.
Kigezo cha kilekisika, hiki ni kiini kingine cha ugumu wa kufasili neno, katika kigezo hiki wataalamu wake hueleza kuwa neno ni kipashio dhahania cha kilekisika ambacho huweza kudhihirika kimaana na kikazi. Kipashio hicho huweza kuwakilishwa kimaandishi au kimatamshi. Cystal (1980) kama alivyo nukuliwa na Mdee anaelezea kuwa leksimu ni kipashio dhahania kinacho wakilisha maumbo kadhaa yanayotokana nacho. Kwa mfano;
                                     refu – ndefu, mrefu, kirefu
                                     baya- baya, mbaya, wabaya
Japokuwa leksimu inaweza kuwa neno si kila leksimu ni neno wala kila neno sio leksimu
Mapungufu ya kigezo hiki,
Swali je, maumbo yanayotokana na leksimu moja kama ilivyo mfano hapo juu ni maneno tofauti au neno moja? Pia kuna maumbo yenye umbo moja lakini maana tofauti, je haya nayo yatakuwa neno moja au maneno zaidi ya moja, kwa mfano;
1.      Paa – mnyama
2.      Paa – enda angani enda juu
3.      Paa – sehemu ya juu ya nyumba
Kigezo cha kisarufi,
Kufasili neno kwa kutumia kigezo hiki nayo ni mojawapo ya kiini cha ugumu wa kufasili neno, kigezo hiki hueleza kwamba neno ni kipashio cha lugha kisicho na maana kubwa lakini huwa na dhima kisarufi. Kazi kubwa ya maneno haya ni kukamilisha maana  kisarufi katika tungo. Mfano katika lugha ya Kiswahili;
a)      Juma ni hodari wa kucheza mpira wa gofu
Hapa maneno “ni” na “wa”, yana maana kisarufi. Mfano Katika lugha ya Kingereza;
b)      A pen, an egg, with spoon, na by bicycle, hapa napo maneno “a” “an” “with” na “by” yana dhima kisarufi.
Upungufu wa kigezo hiki
Kigezo hiki huzingatia dhima zaidi kuliko maana, pia ili neno lijidhihirishe vizuri kidhima ni lazima liwe katika tungo/sentensi.
Kigezo cha maana,
Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa) hueleza kwamba neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana, hueleza zaidi kwamba neno ni lazima liwe na maana. Mfano; baba – mzazi wa kiume, mama – mzazi wa kike. Kwa hiyo kwa kutumia kigezo hiki neno hutambuliwa kuwa ni kipashio cha kiisimu chenye maana
Mapunufu ya kigezo hiki
Je, maneno yote ya luha yana maana ya kisemantiki? Pia kuna maneno mawili au zaidi yenye maana moja, Kwa mfano; mkono wa birika, maana yake mchoyo. Yapo maneno mengine yenye maana zaidi ya moja, mfano; kaa, paa, na kata, maneno haya yakisimama yenyewe huwezi kupata maana moja  mpaka yawe katika mahusiano na maneno mengine kwenye sentensi.
Pamoja na vigezo mbalimbali vinavyotumika kufasili neno kuonekana ndicho kiini cha ugumu wa fasili ya neno lakini pia tofauti za lugha nazo huchangia kufanya fasili ya neno kuwa ngumu. Hii ni kwa sababu tabia za lugha hutofautiana. Pia mitazamo tofautitofauti ya wataalamu nayo ni sababu nyingine ya ugumu huo.
Hitimisho
Kutokana na uwepo wa vigezo vingi vitumikavyo kuainisha maneno, mitazamo tofauti ya wataalamu na kutofautiana kwa tabia ya lugha moja na nyingine, ni vigumu mtu yeyote kutoa maana itakayo kubalika kwa watu wote. Hivyo ili kutoa utata huu ni muhimu vigezo hivi vichanganywe ili kuwa na kigezo kimoja jumui kitakachotumika kutoa fasili ya neno iliyo kamilifu.  Vitu hivi vikizingatiwa vinaweza kupunguza ua kuondoa ugumu wa kufasili neno.

MATEJEO
Katamba, F. (1993) Morphology. Mac Millan Press Ltd, L ondon
Mdee, S. (2010) Nadharia na Historia ya Leksikografia. TUKI, Dar es Salaam
Rubanza. (2010) basic Reading. Yaliyoandailwa na Rubanza.
Spencer, A. (1991) Morhological Theory in Generative Grammar. Congress cataloging, London
TUKI (209). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar es Salaam
TUKI (2010). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar es Salaam


1 comment:

  1. Tungeanza na nyiye katika kutoa maana kulingana na vigezo hivyo vilivyoanishwa na kuchambuliwa

    ReplyDelete