Monday 1 July 2013

TANZU NA VIPERA VYA F. SIMULIZI



Vigezo alivyovitumia Mulokozi katika kugawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi katika Jarida la Mulika (1989) namba 21.
 (Kikosi Kazi)
Kwa mujibu wa Mulokozi katika Mulika namba 21(1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi. Kwa upande wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987)
Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.

Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.
Fasihisi Simulizi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni M.M.Mulokozi (1996) anasema Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.
TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. 
Hivyo basi Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa.
Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila (2003).
Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo, vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)
M.M.Mulokozi katika makala yake ya tanzu za Fasihi Simulizi iliyo katika jarida la Muulika namba 21(1989) amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kwa kutumia vigezo viwili ambavyo ni,kigezo cha kwanza ni umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha pili ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.
Umbile na tabia ya kazi inayohusika: katika kigezo hiki Mulokozi ameangalia vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa hiyo na kuipa muelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna lugha inavyotumika (kishahiri, kinathari, kimafumbo, kiwimbo na kighani), muundo wa fani hiyo na wahusika.
Kwa upande wa muktadha na namna ya uwasilishaji amezingatia kuwa, Fasihi Simulizi ni tukio hivyo huambatana na muingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali. Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua fani fulani ya Fasihi Simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa hadhira, kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika (Mulokozi 1989).
Kwa hiyo kwa kutumia vigezo hivi, Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kama ifuatavyo;
Masimulizi; hii ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha muundo, mara nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile ushairi. Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vilevile kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji. Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.
Masimulizi yamegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisalua (kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano. Ngano (vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha.  Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.
Istiara; hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.
Mbazi; hii ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima.
Kisa; hii ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima.
Utanzu mwingine wa masimulizi ni utanzu wa kisalua. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.
Visakale; haya ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.
Mapisi; haya ni maelezo ya kihistoria bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli.
Tarihi; haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.
Kumbukumbu; haya ni maelezo ya matukio muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambao ni watu.
Visasili; hiki ni kipera kinachofungamana na imani za dini na mizungu ya kajamii pia hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa Semi. Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo. Kigezo kilichotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mkato. Kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambacho ni kufunza.
Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni methali, vitendawili, misimu, mafumbo na lakabu.
Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Vilevile kimetumika kigezo cha muundo ambapo methali huundwa na muundo wa pande mbili ambazo hutegemeana.
Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo.
Misimu; ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Hivyo vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha muktadha yaani hutokea wakati maalum na mazingira maalum.
Mafumbo; ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuonya pamoja na kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.
Lakabu; haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Kigezo kilicho tumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo lugha iliyotumika ni lugha kificho yaani maana yake hufichwa.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.
Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;
Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji, muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada, kilio nakadhalika. Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.
Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.
Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.
Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini.
Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi.
Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.
Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.
Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuomboleza.
Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.
Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini nakadhalika.
Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.
Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto.
Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.
Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.
Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.                
Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.
Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi. Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.
Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.
Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.  
Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.
Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.
Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.
Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.
Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa mazungumzo. Mazungumzo ni maongozi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayalojia.
Utanzu huu wa mazungumzo una vipera vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani, soga, mawaidha na ulumbi.
Hotuba; haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao rasmi au mikutano.
Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.
Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.
Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.
Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.
Utanzu mwingine katika Fasihi Simulizi ni utanzu wa maigizo. Maigizo ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu au wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.
Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa ngomezi. Ngomezi ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kifaa cha uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.
Pamoja na ugawaji huu wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi kwa kuzingatia vigezo vyake alivyovitumia, bado ugawaji huu unaudhaifu mkubwa tu. Udhaifu au changamoto za vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:-
Vigezo vyote hivi vinaweza kuingiliana; mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha huweza kuonekana katika tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali.
Pia kigezo cha namna ya uwasilishaji huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi mwingine. Mfano, katika utanzu wa masimulizi na mazungumzo.
Vilevile kigezo cha wahusika; kigezo hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na mwingine. Mfano, unaweza kuwa na hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo rahisi kuona tofauti zilizopo.  
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kutokana na kwamba, Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.         
MAREJEO:
Mulokozi, M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi: Katika Mulika 21. TUKI. Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.
Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd.                                                       Nairobi.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).

4 comments:

  1. hongera kazi njema lakini mifanano ya fasihi andishi na simulizi ni ipi?

    ReplyDelete
  2. maana ya tanzu ni yaipi? i nipi? na mifanano kati ya fasihi andishi na simuliz

    ReplyDelete
  3. Napenda kuulzi waungwana humu; Hivi hili neno Documentary kwa Kiswahili twaeza kusemaje? Documentary ninayokusudia hapa ni kama ile ya kufuatilia maisha ya wanya, wadudu, au mandhari fulani nk. Amabyo huwa na msimulzi maranyingi mmoja huendeshwa sana kwenye runinga zetu humu kwa Kiswahili na hata kwa Kiingereza.

    naombeni Kiswahili cha neno hilo.
    Shukran

    ReplyDelete