Tuesday 26 November 2013

UFUNDISHAJI LUGHA

UFUPISHO WA SURA YA PILI KATIKA HAMMERLY, H (1982) SYNTHESIS IN SECOND LANGUAGE TEACHING: AN INTRODUCTION TO LINGUISTICS.
LUGHA
Wakati wa vita Waziri Mkuu alikuwa akimalizia hotuba yake bungeni kwa kusema, "Tutakilinda kisiwa chetu kwa gharama yoyote, tutapigana ufukweni, tutapigana nchi kavu, tutapigana milimani, bila kukata tamaa...."Hii ilikuwa ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Winston Churchill tarehe 4.6.1940 bungeni na kuibua ghasia na kila aliyeisikia hataisahau hotuba hii. Mfano huu unaonyesha jinsi lugha inavyojitokeza kuanzia silabi moja mpaka kufikia usemaji wenye ufasaha na kupata waandishi makini.
Lugha ni nini?
Wataalamu mbalimbali wanatofautiana kuhusu maana ya lugha. Kwa karne nyingi wanafalsafa waandishi, wanasaikolojia na wanaisimu wametoa maana mbalimbali za lugha. Tukirejea kwenye Isimu na sayansi ya lugha kuna maana mbalimbali za lugha kama ilivyo Isimu. Kutokana na maana mbalimbali zilizotolewa tunaweza kuwa na maana ya jumla kama ifuatavyo:

“Lugha ni kamilifu, changamani, inabadilika na yenye mfumo nasibu inayotumia alama kwa ajili ya mawasiliano kwa kuzingatia muundo na utamaduni wa jamii husika”
Ifuatayo ni sehemu inayofafanua vipengele 11 vinavyojitokeza katika maana hiyo ya lugha.
Lugha kama mfumo timilifu
Lugha timilifu ni ile inayokidhi mahitaji ya mabadiliko ya mfumo wa jamii na lugha yenyewe. Mwanzoni mwa karne ya 20 Wamisionari na wafanyabiashara walilazimika kutumia lugha ya vitendo, baadaye wakalazimika kutafuta lugha ya mawasiliano kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.
Lugha ni timilifu pale inapokidhi mahitaji ya mawasiliano katika jamii. Misamiati mipya inaweza kuongezeka katika lugha husika kulingana na mahitaji ya jamii kukopa msamiati kutoka lugha nyingine. Pia msamiati huweza kuongezeka katika lugha kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, siasa, uchumi na hata utamaduni. Mfano wa maneno yanayotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni antenna, setilaiti, televisheni na redio.
Uhusiano wa misamiati mbalimbali na mahitaji ya jamii unaonekana vizuri zaidi tunapochukua msamiati toka lugha moja au zaidi na kulinganisha. Mfano huu unaonekana vizuri katika falme za Inca ya zamani huko India (Peru, Bolivia na Ecuador) ambazo zina maneno mengi yanayomaanisha nafaka lakini kwa wazungumzaji wa Kiingereza wana maneno mawili tu.
Kujitosheleza kwa lugha hutegemea sana mahitaji ya mtumiaji. Baadhi ya watu wanajua lugha zaidi kuliko wengine na kujifunza huwa ni kitu kinachoendelea katika maisha ya kila siku.  Mara nyingine lugha haiwezi kujitosheleza kwa mtu na hata jamii, ndiyo sababu nchi zinazoendelea zitaendelea kuwa nyuma kwa matumizi ya misamiati ya kiteknolojia inayotoka katika nchi zilizoendelea. Kwa upande wa mtu binafsi lugha huwa haitoshelezi hususani kwa mtoto mdogo ambaye anashindwa kujieleza na hivyo hutumia ghadhabu na hamaki kutokana na kushindwa kutoa maneno yanayoelezea mahitaji yake.
Matokeo ya kujitosheleza na kutojitosheleza kwa lugha.
  1. Hakuna lugha iliyo bora kuliko nyingine kwa sababu kila lugha hujitosheleza kwa kuzingatia mahitaji ya jamii husika. 
  2. Lugha yoyote inaweza kufundishwa kama lugha ya pili, hivyo ni muhimu kuwa makini kuchagua kipi kifundishwe ili kuifanya lugha ya pili ikamilike kwa mahitaji ya mawasiliano ya mjifunzaji. 
  3. Ili kutowapotezea muda, kutowalazimisha na kutowachanganya, wajifunzaji hawatakiwi walazimishwe kushiriki moja kwa moja kama msingi wa mawasiliano kwa kutumia lugha hiyo haukutolewa. 
  4. Wajifunzaji wakisahau wafundishwe mbinu ya kutumia maneno mengi, ikishindikana mwalimu aeleze ukweli kuhusu maneno waliyoshindwa.
Lugha ni mfumo changamani
Lugha ni mfumo changamani wa mawasiliano unaoundwa na vipande vya sauti zenye maana mbalimbali ambavyo hujitokeza katika miundo tofautitofauti. Miundo hiyo inaunda kipande, neno na maneno ambayo huunda sentensi kamili.Tofauti na lugha za wanyama kama sokwe ambao wana sauti zinazoashiria matukio maalumu, binadamu anaonekana kuwa na mifumo changamani ya lugha kuliko wanyama. Lugha kama mfumo changamani unadokeza vitu viwili;
  • Ujifunzaji wa lugha ya pili huchukua muda mrefu na ni changamani. Hali hii inadhihirisha dhihaka ya madai ya wale wanaofikiri wanaweza kufundisha kwa muda mfupi.
  • Ufundishaji wa lugha ya pili unatakiwa ufuate hatua kwa hatua ili kuzingatia vipengele mbalimbali vinavyofundishwa ili viweze kuleta uhusiano katika mawasiliano. Lugha kama mfumo changamani wenye kanuni na vipengele mbalimbali, mjifunzaji hawezi kujifunza vyote mara moja kwa sababu hakujifunza wakati wa utoto wake.
Lugha hubadilika
Katika hali ya kawaida lugha hubadilika mara kwa mara ingawa baadhi ya sehemu za lugha hubadilika haraka kuliko nyingine. Misamiati ni sehemu ya mabadiliko ya lugha. Mabadiliko ya maana katika lugha hutokea kwa kipindi cha miaka mingi. Baadhi ya misamiati hubadilika maana na mingine hutoweka kabisa. Mfano, katika lugha ya Kiingereza maneno mengi yamebadilika maana. Hata hivyo mabadiliko hayo hayawezi kubadilisha mfumo mzima wa lugha isipokuwa baadhi ya sehemu katika lugha.
Mabadiliko ya kisarufi hujitokeza mara chache kwa muda mrefu na huleta athari katika mfumo mzima wa lugha kuliko msamiati. Mabadiliko ya kifonolojia hutokea mara nyingi. Katika karne ya 18 huko Amerika ya kaskazini matamshi ya / t / na / d / hayakuonesha tofauti ya kimatamshi hususani katika maneno “latter” na “ladder”.
Mabadiliko hayo ya lugha hudokeza mambo manne;
  • Mjifunzaji lugha ya pili kwa ajili ya mawasiliano huhitaji kujifunza miundo na mifumo mipya ya lugha iliyopo. Mfano mjifunzaji akitaka kujifunza Kifaransa na Kiingereza cha sasa hawezi kusoma vitabu vya Chansons de geste na vya Shakespeare kwa sababu lugha inabadilika kihistoria, kiutamaduni na kimaandishi.
  • Data za kihistoria za lugha zinaweza kuonekana kufaa lakini zinaweza zisitumike katika lugha, kwani mfumo wa lugha ya kwanza unaweza usitumike katika kufundishia programu ya lugha ya pili.
Kwa kuwa lugha inabadilika, hata mbinu na vifaa vya kufundishia lazima vibadilike. Lugha iwe inaendana na wakati kwa kuzingatia miundo ya lugha kimazungumzo na kuirekebisha angalau kila baada ya miaka kumi.
  • Mfundishaji wa lugha ya pili anatakiwa ajue mabadiliko na matumizi ya lugha ya kila siku.
Lugha ni  mfumo nasibu
Kuna baadhi ya sifa za lugha ambazo zinajitokeza katika lugha mbalimbali. Mjifunzaji wa lugha ya pili anaweza kuwa mtaalumu wa kujifunza lugha anayojifunza. Katika hali ya kawaida kila lugha ina muundo wake kifonolojia, kimsamiati na upatanisho wa kisarufi ambao unatofautiana na lugha nyingine.
Dokezo kubwa la unasibu katika kujifunza lugha ya pili ni lazima uzingatie msingi wa kifonolojia, kimsamiati na upatanisho wa kisarufi inayotofautiana na mifumo ya lugha ya kwanza ya mjifunzaji. Hata hivyo mjifunzaji wa lugha ya pili anatakiwa kufanya mazoezi kwa kutumia uzoefu alionao kutoka katika lugha yake ya kwanza.  
Lugha ni mfumo
Lugha huwa na mifumo midogomidogo inayohusiana. Sehemu hizo huweza kuwa na umbo au maana, ingawa umbo na maana huenda sanjari. Katika umbo, mifumo midogomidogo ya lugha huhusiana kwa mpangilio wa maneno, uundaji wa maneno, na sauti. Kwa mfano, sehemu za maana ni mifumo midogomidogo ya vinyume vya maneno (Antonimu) kama vile maneno, ndefu / fupi, nene / nyembamba na pana / finyu.
Wanaisimu wameelezea mfumo wa lugha kwa njia nyingi. Wengi wao wametumia mbinu ya Amerika ya kaskazini ambayo ni ya wanaumuundo na wanamabadiliko zalishi. Mbinu hizi zina faida na hasara katika kufundishia lugha ya pili.
Maarifa ya umbo pasipo maarifa ya maana, humfanya mtu asikie neno geni ambalo anaweza kulirudia lakini asielewe kilichomaanishwa. Maarifa ya maana pasipo maarifa ya umbo, msikilizaji anaelewa kwa kutumia muktadha, kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya mzungumzaji au matendo. Hivyo msikilizaji huweza kuelewa kilichomaanishwa lakini hawezi kurudia hata neno moja au zaidi. Hivyo basi, umbo na maana haviwezi kwenda sanjari kwenye kujifunza lugha.
Ufundishaji wa lugha ya pili unahitaji kufanya mazoezi ya kuzungumza kwa kutenganisha umbo na maana katika kurahisisha shughuli ya ujifunzaji. Wafundishaji wengi wa lugha ya pili katika hatua ya kwanza wanaelekezwa kufundisha kwa kufuata mpangilio wa mawasiliano. Ni muhimu katika hatua ya awali kuwahimiza wajifunzaji kujifunza zaidi kwenye misamiati kwa sababu zifuatazo; (a) Misamiati ni muhimu kwa mawasiliano na mambo mengine mjifunzaji anaweza kujifunza nje ya programu. (b) Mfundishaji anatakiwa kuwa makini katika kuchagua msamiati utakaowasaidia wajifunzaji wa lugha ya pili
 Msingi wa lugha ni mazungumzo
Kuna sababu nyingi zinazoeleza kuwa watu wengi hufikiri mtindo wa maandishi katika lugha ndio msingi, na ule wa mazungumzo hufikiriwa katika hali ya kupotoshwa. Sababu hizo zinaeleza kuwa waelimishaji wengi wamejikita katika kutoa elimu, huku watu wengi wakilenga katika kuipata hiyo elimu. Hadi sasa mtindo wa maandishi wa lugha ndio pekee ambao ni imara na wa kudumu. Mambo mengi muhimu ambayo huwashughulisha watu yanahusishwa na nyaraka zilizoandikwa, si nyaraka binafsi za kisheria za mtu bali hata zihusuzo dini (kama vile Biblia na Korani), siasa (Katiba na Ilani za vyama vya siasa) n.k.
Kukwezwa kwa mtindo wa maandishi katika lugha kunatokana na ukweli wake kuwa ndio kinara wa utamaduni, ufahamu na sanaa mathalani fasihi, filosofia, n.k. Lakini ushuhudiaji uliomakinika juu ya asili na matumizi ya lugha unatupeleka katika hitimisho kuwa; “katika jamii za wasomi, mtindo wa lugha ya maandishi na ule wa mazungumzo unahusiana, matamshi ndio msingi wa muundo wa lugha na maandishi yanaegemezwa kwayo.” Baadhi ya fikra zinazotupeleka katika hitimisho hilo ni kama ifuatavyo;
Kwanza, mtazamo wa jumla duniani kote juu ya lugha unaonyesha kuwa, kati ya lugha 3000 ni lugha chache takribani mia ndizo mara nyingi huandikwa. Hivyo lugha ambazo haziandikwi haziwezi kuwa lugha kwa ujumla wake. Pili, kihistoria mtindo wa lugha ya maandishi unaonekana kuwa umeendelea zaidi kuliko ule wa mazungumzo. Hii ni sababu inayoshadidia kuwa mazungumzo ni muhimu zaidi.
Tatu, uzungumzaji hubadilika. Katika lugha nyingi mtindo wa maandishi ulichelewa kwa miongo mingi na karne nyingi ilihali mtindo ule wa mazungumzo ulikuwa tayari umejiimarisha.  Nne, tofauti baina ya mazungumzo na maandishi na ushahidi kuwa mazungumzo ndio msingi unaoweza kudhihirishwa na ukweli kuwa pale lugha zilipopata mabadiliko katika mifumo yake ya maandishi, hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea katika mazungumzo. Mfano mabadiliko yaliyotokea katika Kirumi mwaka 1929.
Tano, lugha huweza kuandikwa kwa namna mbalimbali. Kwa mfano katika lugha ya Kijapani inawezekana kuandika maneno kwa kutumia idiografia (Kanji) au hata kwa kutumia silabi mbili tofauti (Katakana na Hiragana). Hata hivyo lugha ya mazungumzo haiwezi kuundwa kutoka kwenye maandishi kwani lugha ya maandishi sio chimbuko la lugha ya mazungumzo.
Sita, hali ya unyume ilionekana kwamba, lugha mbili au zaidi zinaweza kuandikwa katika namna moja. Yote hii inazidi kutanabahisha uhusiano wa kiutegemezi uliopo baina ya mazungumzo na maandishi. Kwa mfano, idiografia za Kichina zinaweza kusomeka kama maneno tofauti katika Kichina na Kijapani. Mfano huu unafafanua zaidi  λ (“man”)   ni [ ĵεn ] Kichina na [ hi ‘ to ] katika Kijapani.
Saba, kujifunza kuongea lugha mama kwa mtoto mdogo ni jambo la asili (kinasibu) na ni sehemu ya maendeleo katika ung’amuzi na utambuzi wa mtoto. Kwa kawaida mtoto hafundishwi kuzungumza ingawa pindi anapofikia umri wa miaka minne au mitano huwa ameshamudu kuongea lugha hiyo. Kwa upande wa lugha ya maandishi huwa haiwezekani kuielewa kinasibu isipokuwa kwa kufundishwa. Nane, katika kumfundisha mtoto kusoma na kuandika lugha mama, maandishi hutolewa kama kiwakilishi cha lugha ya mazungumzo ambayo mtoto huwa tayari amejifunza. Hii ni sawa na kusema kuwa maandishi huwakilisha lugha ya mazungumzo.
MAREJEO
Hammerly, H. (1982): Synthesis in Second Language Teaching: An Introduction to Linguistics. USA: Second Language Publications.

No comments:

Post a Comment