Saturday 6 July 2013

UFASIHI WA FASIHI


KAZI ZA FASIHI NA ZISIZO ZA FASIHI.
Chunguza vifungu vya habari vifuatavyo:
(a)   Nilipopata barua yako niliumia sana rohoni
(b) Wangu wa moyo nilipopata barua/waraka wako nilihisi uchungu moyoni mithili ya sindano ya moto ipenyayo katikati ya maini. 
(a)  Timu ya Taifa Stars ingefungwa magoli mengi kama si uhodari wa Kaseja.
(b) Kaseja ni nyani kweli kweli, kama si yeye mlango wa Taifa Stars ungekuwa kapu la magoli.
Vifungu “a” vinafanana na vifungu “b” kimantiki. Utofauti wake upo katika ufundi wa uchaguzi wa lugha iliyotumika. Hivyo kufanya vifungu b vionekane wazi kuwa ndiyo kazi ya kisanaa kwani vimeongezwa viungo vya ustadi mkubwa wa lugha na kupagwa inavyostahili. Ufundi na ustadi huo wa lugha unaleta mvuto na mnato kwa msomaji/msikilizaji.

Sanaa ya uumbaji maneno ili kuleta uzuri ndio huitwa Fasihi. Sanaa hii hujionesha kwa namna mbalimbali ya kueleza jambo, yaani inaweza ikafichwa kwa fumbo, shairi, kitendawili, tamthiliya au hadithi. Mara nyingine taarifa haifichwi ila inaelezwa kwa lugha ya mkato. “Mpanda ngazi hushuka” badala ya kusema mtu anayepanda ngazi kuna wakati atalazimika kuteremka.
Sanaa ya lugha inaleta uhai na kuongeza mvuto. Lugha inaweza kupewa uhai huu kwa kutumia tamathali za usemi kama vile: tashbiha, sitiari, tashihisi, tafsida, nk. Pia vipengele vingine vinavyotawala fasihi ni uumbaji wa wahusika, uchoraji wa mandhari, matumizi ya picha na utendaji.
Kazi ya fasihi mara nyingi ni za mficho zikiwa na lengo hasa la kuchochea na kuhamasisha au kuamsha ari ya kutafuta kilicho ndani. Zina umbo la nje na ndani.
MAANDISHI YA KAWAIDA
Haya ni maandishi ya kawaida ambayo hayatumii usanii na ustadi. Maandishi haya hayatumii viungo vya lugha kama vile tamathali za semi. Maandishi ya kawaida hufuata kanuni za lugha sanifu ambazo hutoa maana moja kwa moja.
Maandishi haya hupatikana katika matangazo mbalimbali, vitabu vya masomo mbalimbali mfano; Jiografia, Historia, Kemia, Siasa; pia katika semina, makongamano ya kitaaluma nk.
Maandishi haya hayana ufundi na ustadi au usanii, ukiachilia mbali usanifu wa lugha yake. Lugha inayotumika ni kavu na haina pambizo.
Kwa maelezo hayo yote tunaweza kusema kwa kifupi kuwa

MAANDISHI YA KIFASIHI

MAANDISHI YA KAWAIDA
1
Yana umbo la nje na la ndani
1
Yana umbo la nje tu.
2
Lugha itumikayo ni ya kisanii
2
Lugha itumikayo haina usanii wowote
3
Hutumia tamathali za semi
3
Huwa kavu na sanifu
4
Hutumia lugha ya mficho
4
Ni lugha ya kawaida na ya wazi
5
Msomaji huvutwa na mambo mengi mfano: muundo, mtindo, wahusika, visa, nk.
5

Hayana mambo mengi jambo liongelewalo ni hilo hilo.
6
Matumizi ya lugha ni mapana. Mfano: kuchanganya lugha za kigeni km vile; Kiingereza, picha, lugha za mitaani, taswira, ishara nk.




Lugha itumikayo hufuata kanuni za lugha – lugha fasaha na sanifu tu.
7
Kuna matukio ya kubuni
7
Matukio huwa ni halisi na pengine huwa yamefanyiwa utafiti.
8
Wahusika huumbwa kisanii na ni vipaza sauti vya maisha halisi ya watu na mazingira.
8
Wahusika huwa ni halisi

DHIMA YA FASIHI
-         Kuelimisha.
-         Kuburudisha.
-     Kuasa na kutahadharisha jamii juu ya mambo yanayojitokeza  katika maisha.
-     Kupiga vita maovu na mazingira ya umasikini, ujinga, njaa na maradhi
-         Kutiisha na kukosoa vipengele mbalimbali vya maisha
-         Kutunza historia hususani kwa fasihi simulizi
-         Kutia hamasa kwa upande wa ushairi

UMUHIMU WA KUJIFUNZA FASIHI

1. Kwa vile Fasihi inahusu maisha ya binadamu hivyo inamwelekeza mwanadamu kufichua ukweli wa mambo ulivyo na pia kupanua mawazo kutokana na maisha ya watu wengine.
2.     Kuamsha udadisi na hamu ya kuwaelewa watu wengine na sisi wenyewe.
3.  Kueleza na kudumisha urithi wa utamaduni wetu/kutambulisha utamaduni wa jamii husika.
4.  Kutokana na fasihi kuwa maelezo ya kisanaa hivyo kuna mwezesha mtu kuona njia na mitindo mbalimbali ya kujieleza.
5.  Kama burudani, kutokana na kuwa fasihi ina mvuto maalum katika lugha, muundo na maudhui.
6.   Kumsaidia mtu katika kujenga msimamo mpya kulingana mahitaji ya jamii kwa wakati huo.
DHIMA YA MWANAFASIHI.
Jukumu la mwanafasihi katika jamii ni kama vile;
1. Kuelimisha – kufichua ukweli wa mambo ulivyo juu ya maisha ya mwanadamu na kupanua mawazo ya watu wengine kutokana na watu wengine.
Mfano katika DIWANI YA MWENYE MACHO shairi la "Niwapi Tumekosea?" Mshairi anaizindua jamii kwa kusema:

                    "Maisha bora ya wapi, ari mpya nayo ipi!
Na kasi mpya i wapi, na nguvu mpya ni ipi!
Mkukuta uko wapi, mkurabiti ni vipi!
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?

                    Misitu yatulilia, wanyama wanapotea,
Madini yana pepea, hakuna wa kuzuia,
Tumepuuza wosia, hamnazo kujitia,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?

                    Aridhi wametoboa, fuko wamewachukua,
Mashimo yamebakia, urithi wa vizalia,
Laana ya ng’ang’ania, kizazi hata vizazi,
Yangu hoja inahoji, NI WAPI TUMEKOSEA?"
2.  Kuamsha udadisi na hamu ya kuwaelewa watu wengine na wao wenyewe pia
3.   Kuendeleza na kurithisha na kuhifadhi urithi wa utamaduni wa jamii.
4.  Kuburudisha jamii, kwani fasihi ina ladha na mvuto maalum katika lugha, mtindo na mandhari yake.
5.  Kuelezea njia na mitindo mbalimbali ya kujieleza kisanii na kwa njia hii kunaelekeza watu kuwa wanafasihi.
6.  Kuwajenga watu kifikra na kisiasa pia kiuchumi. Hii inamsaidia mtu kujenga msimamo mpya kulingana na mahitaji yake na ya jamii yake. 
7.  Kujenga tabia, kuasa yaani kuonya au kutoa maadili. Fasihi ina dhima ya malezi kwa watoto na maonyo kwa watu wazima.
8.     Kueleza harakati za jamii dhidi ya mazingira
9. Kujenga utaifa: Fasihi inasaidia kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa makabila mbalimbali yanaunda “mataifa” huru ya Afrika (Sengo na Kiango 1978:8-9)

2 comments:

  1. Tunaweza kupata topic ya usanifu wa maandishi kwa ajili ya Alevel

    ReplyDelete
  2. habari wadau wa kiswahili , kama alivotangulia mwenzangu hivi tunaweza kupata topic ya usanifu wa maandishi kwa a level

    ReplyDelete